Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

DKT. KIDA AKUTANA NA UJUMBE KUTOKA BENKI YA MAENDELEO YA KIMATAIFA YA JAPAN (JBIC)


Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida, amefanya mazungumzo na ujumbe kutoka Benki ya Maendeleo ya Kimataifa ya Japan (JBIC), jijini Dar es Salaam.

Mazungumzo baina ya Dkt. Kida na ujumbe huo kutoka Japan yalilenga kupata uelewa wa sera za Tanzania za kuvutia uwekezaji na kuimarisha mazingira ya biashara.

Ujumbe wa JBIC, wa taasisi hiyo ya kifedha iliyo chini ya Wizara ya Fedha ya Japan, ulimweleza Dkt. Kida kuwa lengo lao ni kuhamasisha kampuni za Kijapan kuwekeza Tanzania, hivyo pamoja na mambo mengine wanahitaji uhakika wa sera thabiti na mazingira bora ya kufanya biashara.

Katibu Mkuu aliwakaribisha ujumbe huo, akiwashukuru kwa ushirikiano wa muda mrefu wa Japan kupitia shirika lake la maendeleo la JICA katika sekta mbalimbali nchini Tanzania.

Dkt. Kida amewafahamisha kuhusu jitihada za Serikali za kuimarisha uchumi na kuvutia uwekezaji, akijumuisha utekelezaji wa Blueprint, Sera mpya ya uwekezaji ya mwaka 2022, na maboresho katika mashirika ya umma.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.