Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

DKT. KIDA ARIDHISHWA NA MAENDELEO YA UJENZI WA JENGO LA OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI.


Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Dkt. Tausi Kida amepongeza jitihada zilizofanywa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi kwa kushirikiana na wataalamu walio chini yake kwa kusimamia vizuri ujenzi wa jengo hilo ambalo kwa sasa limefikia asilimia 54 kukamilika.

Dkt. Kida ameyasema hayo leo tarehe 17 Julai, 2024 wakati wa hafla ya makabidhiano ya nyaraka 18 kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na uratibu kwenda Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji ili kuendelea na usimamizi wa ujenzi wa jengo linalojengwa na mkandarasi Suma JKT Kanda ya kusini katika mji wa Serikali Mtumba, Dodoma.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi amepongeza kazi kubwa inayofanywa na Katibu Mkuu Dkt. Kida kwa kufanya ufuatiliaji wa karibu uliopelekea kufanikisha makabidhiano kwa Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kuendelea kusimamia jengo hilo.

Dkt. Yonazi ameongeza kuwa jengo hilo litakuwa na vyumba 116 kwa ajili ya maafisa, ukumbi wa mikutano wenye uwezo wa kuchukua watu 155, kumbi ndogo sita za mikutano zenye uwezo wa kuchukua watu 25 kila mmoja, chumba cha madereva, vyumba vya kuhifadhia nyaraka, chumba cha maktaba, TEHAMA, Ofisi ya walinzi, mapokezi na eneo la maegesho ya magari.

Naye mshauri elekezi wa mradi Bw. Saudeni Anania kutoka kampuni ya ABECC amesema kuwa ujenzi wa jengo hilo la Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji umefikia asilimia 54 ambapo unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba, 2024.