Habari
SEKTA YA VIWANDA KUONDOA UTEGEMEZI KUELEKEA DIRA 2050
Katika maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 Serikali inalenga kuweka vipaumbele vyake katika maendeleo ya viwanda kwa lengo la kuondoa utegemezi wa kununua bidhaa nyingi nje ya nchi.
Hayo yamesemwa leo tarehe 23 Julai, 2024 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Profesa Kitila Mkumbo (Mb.), wakati akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa viwanda.
Katika mkutano huo ulioandaliwa na Shirikisho la Wenye Viwanda (CTI), Mheshimiwa Prof. Mkumbo alishuhudua uzinduzi wa tuzo za Rais za Mzalishaji Bora Viwandani PMAYA ambazo hufanyika kila mwaka kwa wenye viwanda.
Akichambua mitazamo mbalimbali kuhusu maendeleo, Mhe. Profesa Mkumbo alisema kuwa maandiko ya wanazuoni mbalimbali hutizama tofauti kati ya nchi tajiri na zile maskini kwa idadi ya viwanda, kwamba nchi tajiri huwa na viwanda vingi wakati maskini hazina viwanda na zinategemea kununua bidhaa nje ya nchi.
“Itakuwa vigumu sana kutengeneza Dira ya Taifa bila kuweka viwanda katikati ya dira hiyo kwa sababu hilo ni la msingi na tafiti nyingi zinaonesha kuwa hatuwezi kuendelea kwa kununua bidhaa nje ya nchi, lazima tuwe na viwanda vingi tuuze nje,” amesema Prof. Mkumbo.
Prof. Mkumbo ameongeza kuwa katika utafiti ambao umefanywa na serikali katika maandalizi ya dira hiyo uliohusisha watu 7,668 nchi nzima waliochaguliwa kisayansi walitaka vipaumbele vitano kutiliwa mkazo kwenye dira hiyo.
Alitaja Viwanda kama miongoni mwa vipaumbele vilivyotajwa na wananchi waliotoa maoni wakisema kuwa asilimia 65 ya malighafi zinazotumika viwandani zinatokana na kilimo hivyo kilimo nacho kitaendelea kuwa kipaumbele kwenye dira hiyo.
Alisema kipaumbele kingine kilichotajwa kwenye utafiti huo ni uwekezaji mkubwa kwenye rasilimali watu kwani uchumi wa viwanda unahitaji watu waliosoma vizuri.
“Lazima dira yetu ituelekeze kuwekeza kwenye elimu na siyo elimu tu bali elimu iliyo bora,” alisema Profesa Mkumbo.