Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji

Habari

VIJANA WANAONGOZA KUTOA MAONI DIRA YA TAIFA 2050


Takwimu za maoni ya wanachi yaliyokusanywa kuhusu Dira Taifa ya Maendeleo 2050 ziaonesha kuwa idadi kubwa ya wananchi waliofikiwa na timu ya kuchukua maoni ni vijana wenye umri kati ya miaka 15-35 sawa na asilimia 81 ya watu wote waliotoa maoni kuhusu dira hiyo.

Hayo yameelezwa na Mheshiwa Prof. Kitila Alexander Mkumbo (Mb.), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji alipokuwa akitoa taarifa ya mchakato wa kuandika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwenye Kongamano la kwanza la Kikanda linalofanyika leo jijini Mwanza.

“Data hizi zinaakisi uhalisia kwamba asilimia 75 ya Watanzania ni vijana, na kwa kweli ni jambo jema kwa kuwa miaka 25 ijayo hawa ndio watakuwa na dhamana kubwa katika taifa letu” Amesema Prof. Mkumbo.

Aidha, Mheshimwa Prof. Mkumbo amesema kuwa, njia mbalimbali za kutoa maoni zikihusisha kupokea ujumbe kwa njia ya simu, kupiga simu, tovuti mahususi, utafiti, mahojiano ya ana kwa ana, zimetumika ili kuhakikisha kwamba idadi kubwa ya wananchi wanashiriki na kuwa sehemu ya mchakato wa kuandika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“ Tumeamua kutumia njia mbalimbali, kwa sababu pamoja na kwamba Dira 25 ilikuwa na mafaniko ni watu wachache waliotoa maoni yao, mathalani ni asilimia 22 pekee ya watu waliotoa kwa njia ya tovuti wamewahi kusikia kuhusu Dira 2025, na asilimia 35 ya waliotoa maoni kwa njia ya kupiga simu wamewahi kuisikia” amesema Mhe. Prof. Kitila Mkumbo.

Vile vile, Mheshimiwa Prof. Mkumbo ameeleza baadhi ya mambo yaliyojitokeza katika tathimini ya Dira ya Taifa 2025, ambayo imeonesha kuwa asilimia 69 wanaamini nchi iko katika muelekeo sahihi, huku asilimia 76 wakiamini kuwa miaka 25 mbele nchi itakuwa na ustawi mkubwa zaidi.

Wakati huo huo, maoni mengi yanayochukuliwa kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yanaonesha kuwa wananchi wengi wanataka kuona uchumi na ustawi wa jamii vikikuwa zaidi.