Habari
MHE. PROF. MKUMBO AELEZA MAFUNZO MUHIMU NORWAY IKIADHIMISHA MIAKA 211

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, alieleza kuwa Tanzania inaweza kujifunza mengi kutoka kwa misingi imara ya utawala bora, usawa, na maendeleo endelevu ya Norway katika safari yake kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Mhe. Prof. Mkumbo alitoa kauli hiyo Mei 16, 2025 jijini Dar es Salaam alipokuwa akitoa hotuba yake katika maadhimisho ya miaka 211 ya Siku ya Katiba ya Norway na kuishukuru nchi hiyo kwa kuendelea kuwa mshirika wa kweli wa Tanzania katika ajenda ya maendeleo katika maeneo mengi.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuimarisha taasisi za kidemokrasia, uwajibikaji, na usimamizi endelevu wa rasilimali, akitolea mfano mafanikio ya Norway katika sekta ya nishati.
Prof. Mkumbo aliongeza kuwa uwekezaji katika rasilimali watu na ushirikiano wa kimataifa ni muhimu katika kufikia malengo ya TDV 2050.
"Tunajifunza kutoka Norway jinsi ya kujenga taifa lenye ustawi kwa kuweka misingi imara ya utawala na kutumia rasilimali zetu kwa manufaa endelevu," alisema Prof. Mkumbo, akionyesha umuhimu wa ushirikiano unaoendelea kati ya Tanzania na Norway katika kufikia malengo ya maendeleo.
Kwa upande wake Balozi wa Norway nchini Tanzania, Mhe. Tone Tinnes ameeleza kuwa nchi yake itaendelea kuimarisha ushirikano wa kibiashara na uwekezaji katika sekta mbalimbali.